Wanaharakati wazindua juhudi za kupinga ubaguzi kwa ajili ya kuitenga Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119536-wanaharakati_wazindua_juhudi_za_kupinga_ubaguzi_kwa_ajili_ya_kuitenga_israel
Muungano wa watu mashuhuri kutoka kote duniani umezindua sura ya Afrika Kusini ya harakati ya kupinga ubaguzi wa rangi dhidi ya Israel.
(last modified 2024-11-30T08:31:46+00:00 )
Nov 30, 2024 08:31 UTC
  • Wanaharakati wazindua juhudi za kupinga ubaguzi kwa ajili ya kuitenga Israel

Muungano wa watu mashuhuri kutoka kote duniani umezindua sura ya Afrika Kusini ya harakati ya kupinga ubaguzi wa rangi dhidi ya Israel.

Baada ya mkutano wake wa kwanza wa kimataifa uliofanyika mwezi Mei mjini Johannesburg, harakati ya kupinga ubaguzi (apartheid) dhidi ya Israel sasa imeanza juhudi mpya za kimataifa zinazokusudia kuutenga utawala wa Kizayuni na ulimwengu uliostaarabika.

Mpango huo umeshuhudia ushiriki wa wawakilishi wa serikali, wanaharakati, wanasheria na makundi ya kiraia kutoka duniani kote.

Akiashiria uzinduzi wa mpango huo, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, amesema kuwa Israel lazima isitishwe.

Kwa upande wake, Mchungaji Frank Chikane, mratibu wa vuguvugu la kimataifa la kupinga ubaguzi wa rangi, amesisitiza ukweli kwamba Israel inashikilia mambo mawili ambayo yamesababisha mateso makubwa duniani kote; ubaguzi wa rangi na fikra za kikoloni.

Pia ameyalaumu mataifa ya Magharibi kwa kuendelea kuipatia silaha Israel, jambo ambalo linawezesha mashambulizi yake ya kikatili. 

Wanaharakati wanasema serikali ya Afrika Kusini inasuasua katika kuwafungulia mashtaki Waafrika Kusini ambao wameshirikiana na jeshi la Israel katika mauaji ya watu wa Gaza.

Mjukuu wa Mzee Nelson Mandela, shujaa wa mapambano ya uhuru wa Afrika Kusini, Zwelivelile “Mandla” Mandela, amesema: "Tunapongeza hatua zilizochukuliwa na serikali yetu katika kesi dhidi ya Israel katika mahakama ya ICJ, tunapaswa kulize swali kwamba, kwa nini wahalifu hawa bado wanatembea huru kwenye mwambao wetu. Kwa nini hawajakamatwa?

Zwelivelile “Mandla” Mandela

Katika ngazi ya kimataifa, Mandla Mandela amekuwa akipaza sauti yake na kutoa wito wa kufukuzwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa.