Karibu watu 27 wafa maji baada ya boti kuzama, Nigeria
Karibu watu 27 wamekufa baada ya boti kuzama katika Mto Niger, katikati mwa Nigeria.
Msemaji wa Idara inayosimamia masuala ya dharura kwenye jimbo la Kogi, Sandra Musa amesema, idadi jumla ya watu waliokufa itatolewa baada ya zoezi la uokozi kufungwa.
Amesema hadi sasa miili 27 imepatikana kufuatia ajali hiyo iliyotokea siku ya Alhamisi usiku na kazi ya kuwasaka wahanga inaendelea.
Boti hiyo kwa kiasi kikubwa ilikuwa imewabeba wafanyabishara wa jamii ya Missa, jimbo la Kogi waliokuwa wakielekea kwenye soko la wiki katika jimbo jirani la Niger na hawakuwa wamevaa vifaa vya kujiokoa, hali iliyosababisha wengi kuzama majini.
Mwezi Oktoba mwaka huu pia, polisi ya Nigeria ilithibitisha kupoteza maisha takriban watu 21 baada ya boti mbili za abiria ambazo hazikuwa zimesajiliwa kupinduka. Boti hizo zilipinduka baada ya kugongana katika jimbo la Lagos.
Aidha Septemba mwaka huu, watu wasiopungua 64 waliaga dunia katika ajali ya boti iliyotokea mtoni katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.