Tunisia yasambaratisha mitandao miwili ya magendo ya mihadarati karibu na mji mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119574-tunisia_yasambaratisha_mitandao_miwili_ya_magendo_ya_mihadarati_karibu_na_mji_mkuu
Vikosi vya usalama vya Tunisia vimesambaratisha mitandao miwili ya magendo ya dawa za kulevya katika majimbo ya Ben Arous na Ariana karibu na mji mkuu wa Tunis.
(last modified 2024-12-01T08:02:46+00:00 )
Dec 01, 2024 08:02 UTC
  • Tunisia yasambaratisha mitandao miwili ya magendo ya mihadarati karibu na mji mkuu

Vikosi vya usalama vya Tunisia vimesambaratisha mitandao miwili ya magendo ya dawa za kulevya katika majimbo ya Ben Arous na Ariana karibu na mji mkuu wa Tunis.

Radio ya Taifa ya Tunisia imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, vitengo vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kusambaratisha magenge hayo katika operesheni mbili tofauti na kuwatia mbaroni watu tisa na kukamata kiasi kisichojulikana cha dawa za kulevya, pesa na gari.

Ripoti hiyo haikutaja ni lini zimefanyika operesheni hizo wala uraia wa watu waliotiwa mbaroni lakini imethibitisha kuwa wawili ya watuhumiwa hao walikuwa wakisakwa kwa tuhuma mbalimbali.

Serikali ya Tunisia imechukua msimamo mkali dhidi ya magendo ya mihadarati na dawa haramu za kulevya. Hivi karibuni Tunisia imeanzisha operesheni kabambe za nchi nzima na kufanikiwa kukamata mamia ya watu wanaojihusisha na magendo ya madawa ya kulevya.

Mbali na magendo ya madawa ya kulevya, katikati ya mwezi ulioisha wa Novemba, Walinzi wa Taifa wa Tunisia walitangaza kuwa wamesambaratisha mtandao wa magendo ya binadamu unaohusika na kusafirisha wahamiaji wasio na vibali.

Walinzi hao walisema kuwa, operesheni hiyo iliendeshwa katika jimbo la Ben Arous karibu na mji mkuu Tunis baada ya kupatikana taarifa za kiintelijensia za kuweko mtandao unaosafirisha wahamiaji wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara la barani Afrika wasio na vibali.

Tunisia, iko kwenye ncha ya kaskazini mwa Afrika na inaendelea kuwa kituo kikuu cha uhamiaji haramu kuelekea barani Ulaya.