Misri: Tuko pamoja na Syria katika kupambana na magenge ya kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119578-misri_tuko_pamoja_na_syria_katika_kupambana_na_magenge_ya_kigaidi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza kuwa nchi hiyo iko pamoja na serikali na wananchi wa Syria katika kupambana na magenge ya kigaidi.
(last modified 2024-12-01T08:03:40+00:00 )
Dec 01, 2024 08:03 UTC
  • Misri: Tuko pamoja na Syria katika kupambana na magenge ya kigaidi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza kuwa nchi hiyo iko pamoja na serikali na wananchi wa Syria katika kupambana na magenge ya kigaidi.

Shirika la habari la FARS limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty amefanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria kuhusu uvamizi na mashambulio ya genge la kigaidi na ukufurishaji la Jabhatun Nusra (Tahrir al Sham) dhidi ya mikoa ya Edlib na Halab ya Syria na kusisitiza kuwa Cairo iko pamoja na wananchi na serikali ya Syria katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilitoa tamko jana na kusema kuwa, katika mazungumzo ya mawaziri hao wa mambo ya nje wa Misri na Syria, pande mbili zimetilia mkazo wajibu wa kushirikiana kupambana na magenge ya kigaidi na kuheshimiwa haki ya kujitawala ardhi yote ya Syria.

Jumatano iliyopita, magenge ya kigaidi yaliyoko katika mkoa wa Idlib wa Syria na hususan genge la ukufurishaji la Jabhatun Nusra yalifanya mashambulizi makubwa dhidi ya vijiji na miji ya mkoa wa Halab wa kaskazini wa magharibi mwa Syria na kuteka baadhi ya maeneo ya mkoa huo.

Kabla ya hapo nchi kadhaa zikiwemo Iran, Russia, Imarati na Iraq zimetangaza rasmi kuwa ziko pamoja na wananchi na serikali ya Syria katika kupambana na magenge ya kigaidi na Kizayuni na kulinda haki ya kujitawala ardhi nzima ya Syria.