Marais wa Kenya na Uganda kupatanisha mzozo wa Somalia na Ethiopia
Marais wa Kenya na Uganda wanatarajiwa kuwa wapatanishi wa mzozo wa Ethiopia na Somalia ambao umetishia kuzitumbukiza nchi hizo katika mgogoro mkubwa wa kidiplomasia.
Rais wa Kenya William Ruto amesema, yeye na Rais wa Uganda Yoweri Museveni watasaidia kupatanisha Ethiopia na Somalia katika mzozo unaotishia kuvuruga ukanda wa Pembe ya Afrika.
Rais Ruto amesema kwamba, ni jukumu la pamoja la viongozi wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha kwamba, kanda nzima ina usalama na utulivu.
Amefichua kwamba Kenya na Uganda zitaongoza juhudi za mazungumzo kati ya Ethiopia na Somalia ambazo zimekuwa katika mzozo wa kidiplomasia unaotishia utulivu katika eneo hilo.
Ethiopia isiyo na bandari, ambayo ina maelfu ya wanajeshi nchini Somalia kupambana na waasi wenye mafungamano na al Qaeda, imeikasirisha serikali ya Mogadishu kwa mpango wake wa kujenga bandari katika eneo lililojitenga la Somaliland.
Somaliland, ambayo badala ya bandari hiyo inaweza kupata kutambuliwa kama taifa huru kutoka Ethiopia, imejitahidi kupata kutambuliwa kimataifa licha ya kujitawala na kufurahia amani na utulivu linganishi tangu kujitangazia uhuru wake mwaka 1991.
Mzozo huo umeifanya Somalia kuwa karibu na Misri, ambayo imekuwa ikizozana na Ethiopia kwa miaka mingi juu ya ujenzi wa Addis Ababa wa bwawa kubwa la maji kwenye Mto Nile, na Eritrea, adui mwingine wa Ethiopia.