Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waijadili DRC
Viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamefanya juhudi kwa mara nyingine tena za kujaribu kuleta amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Viongozi hao waliokutana jana Jumamosi bado walishindwa kupiga hatua kufuatia kutokuwepo kwa Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo na kuondoka mapema kwa mwenzake wa Rwanda Paul Kagame katika mkutano huo wa kilele wa kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Taarifa iliyosomwa mwishoni mwa mkutano huo wa faragha mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania ilisema tu kwamba kuna haja ya kuzijumuisha pamoja juhudi zote za kutafuta amani ya kudumu Mashariki mwa Kongo. Rais Paul Kagame aliondoka muda mfupi baada ya mkutano huo lakini hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu kutoshiriki kwa Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Salva Kiir wa Sudan Kusini, Mama Samia Suluhu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, William Ruto wa Kenya,Yoweri Museveni wa Uganda na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia..