Umoja wa Mataifa wataka kushughulikiwa mgogoro wa Sudan
Mkuu wa masuala ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa Jamii ya Kkimataifa kuchukua hatua za haraka ili kushughulikia mzozo wa Sudan unaozidi kuwa mbaya.
Tom Fletcher amesisitiza kuwa, mateso ya mamilioni ya watu waliokoseshwa makazi kutokana na mzozo huo yanazidi kuongezeka.
Tom Fletcher alizungumza na wakimbizi wakati wa ziara ya siku tisa nchini Sudan na Chad, akiapa kupaza sauti zaidi kwa kuwatetea na kuutaka ulimwengu kutoa msaada mkubwa zaidi.
Wakati huo huo, mapigano makali yameripotiwa kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika miji kadhaa ya Sudan, huku idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao ikiendelea kuwasili katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa jeshi kaskazini mwa nchi hiyo.
Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala, na kundi la RSF linaloongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 12,260 wameuawa na zaidi ya 33,000 kujeruhiwa katika vita vilivyoanza Aprili 2023,
Mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya zaidi kwani karibu watu milioni 6.8 wamekimbia makazi yao kutafuta usalama nchini Sudan au nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa hadi sasa ziimeshindwa kukomesha mapigano hayo.