DRC kuishtaki Rwanda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119648-drc_kuishtaki_rwanda_mahakama_ya_afrika_ya_haki_za_binadamu_na_watu
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa inaendelea na kesi dhidi ya nchi jirani ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na Watu, ambayo ni mamlaka iliyo chini ya Umoja wa Afrika yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania.
(last modified 2024-12-03T03:46:31+00:00 )
Dec 03, 2024 03:46 UTC
  • DRC kuishtaki Rwanda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa inaendelea na kesi dhidi ya nchi jirani ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na Watu, ambayo ni mamlaka iliyo chini ya Umoja wa Afrika yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania.

Samuel Mbemba, Naibu Waziri wa Sheria wa DRC amesema kuwa, kesi hiyo itasikilizwa tarehe 12 Februari 2025 kuhusu mauaji na uporaji uliofanyika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha amersema, "kwa miongo kadhaa ya uchokozi dhidi ya nchi yetu, uporaji wa madini yetu, ubakaji wa watoto wetu na wanawake wetu, na mauaji ya watu wetu, Rwanda na Paul Kagame hawajawahi kufunguliwa mashtaka kwa kesi za kweli."

Mkutano wa kilele wa pande tatu, Angola-Rwanda-DRC, utafanyika Luanda mnamo Desemba 15, 2024, chini ya usimamizi wa Rais wa Angola João Manuel Gonçalves Lourenço, mpatanishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika katika mzozo wa mashariki mwa DRC.

Mkutano huo unatarajiiwa kuwaleta pamoja Marais Félix Tshisekedi wa DRC, Paul Kagame wa Rwanda, na mwenyeji wao wa Angola, ili kuharakisha juhudi za kuleta amani na utulivu katika eneo la Maziwa Makuu linalokumbwa na ghasia.