Watu 79 wafariki dunia kwa "ugonjwa usiojulikana" kusini magharibi mwa DR Congo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119678-watu_79_wafariki_dunia_kwa_ugonjwa_usiojulikana_kusini_magharibi_mwa_dr_congo
Takriban watu 79 wamefariki dunia kutokana na "ugonjwa ambao bado haujajulikana asili yake" na ambao unaoendelea kuenea katika jimbo la Kwango la kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2024-12-03T23:58:54+00:00 )
Dec 03, 2024 23:58 UTC
  • Watu 79 wafariki dunia kwa

Takriban watu 79 wamefariki dunia kutokana na "ugonjwa ambao bado haujajulikana asili yake" na ambao unaoendelea kuenea katika jimbo la Kwango la kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na mamlaka husika mapema leo Jumatano alfajiri na kuongeza kuwa, timu maalumu ya kukabiliana na ugonjwa huo imepelekwa kwenye eneo hilo ili kubaini aina ya ugonjwa huo ambao unaaminika ni wa kuambukiza, na kuwataka wananchi kuepuka mikusanyiko ya watu wengi.

Dalili za ugonjwa huo mpya ni homa kali, maumivu ya kichwa, matatizo katika mfumo wa mapafu na kupumua pamoja na upungufu wa damu.

Remy Saki, makamu wa mkuu wa mkoa huo wa Kwango wa kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amenukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema kuwa kati ya vifo 67 hadi 143 vilikuwa vimesharekodiwa hadi kufikia jana Jumanne kutokana na ugonjwa huo.

Mbali na magenge ya waasi na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanateseka pia kwa miripuko ya mara kwa mara ya magonjwa hatari, yakiwemo magonjwa yasiyojulikana.