Wasiwasi watanda baada ya ndege ya kijasusi ya Marekani kuonekana Uganda, DRC
Ndege ya kujasusi ya Marekani inachunguzwa baada ya kukiuka anga ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mara kadhaa mwezi Novemba.
Ndege ya Bombardier Challenger 604, iliyotambuliwa kama N9191 na yenye makao yake Djibouti, ilifanya safari tatu za ndege katika eneo hilo mnamo Novemba 14, 15, na 26, na huku kukiwa na wasiwasi kuwa inatekeleza opereseheni za kijasusi
Kwa mujibu wa gazeti la Kampala Pos, serikali ya Uganda hapo awali ilikuwa imeidhinisha kuruka kwa ndege hiyo, kufuatia oombo la Mwambata wa Kijeshi wa Marekani mjini Kampala kwa ajili ya kusafirisha wafanyakazi na vifaa hadi DRC. Hata hivyo, maafisa wa rada wa Uganda waliashiria mwelekeo usio wa kawaida wa ndege karibu na maeneo nyeti, ikiwa ni pamoja na vituo vya kijeshi na vituo vya uzalishaji wa mafuta katika eneo la Albertine. Ndege hiyo haikutua DRC kama ilivyotarajiwa, jambo linalozidisha wasiwasi.
Kufuatia uchunguzi huu, Mkuu wa Majeshi ya Uganda alibatilisha vibali vya ndege hiyo kuruka katika anga ya nchi hiyo. Safari ambazo hazikuidhinishwa za ndege hiyoa pia zimewakasirisha maafisa wa DRC, ambao waliwatahadharisha viongozi wakuu wa Uganda, akiwemo Rais Museveni.
Kamandi ya Jeshi la Marekani Afrika, AFRICOM, imekiri kwamba ndege hiyo "iliondoka katika mkondo wake ulioidhinishwa" lakini imekanusha taarifa kuwa ilikuwa katika operesheni maalumu za ujasusi. Uwezo wa juu wa kijasusi wa wa ndege hiyo na uhusiano na wakandarasi wa kijasusi wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Tenax Aerospace, umeibua maswali kuhusu dhamira yake ya kweli.
Siku ya Jumanne, Mbunge wa Uganda Ibrahim Ssemujju alitaka maelezo kuhusiana na uhusiano wa Uganda na Marekani kufuatia madai ya ukiukaji wa anga.