Iran yahimiza juhudi za kidiplomasia kukabiliana na tishio kubwa la ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119736-iran_yahimiza_juhudi_za_kidiplomasia_kukabiliana_na_tishio_kubwa_la_ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ametahadharisha kuwa, kuibuka tena ugaidi nchini Syria na kuenea kwake katika eneo kutaleta tishio kubwa kwa amani, utulivu na usalama na hivyo ametaka kuwepo juhudi kukabiliana na tishio hilo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 05, 2024 04:27 UTC
  • Iran yahimiza juhudi za kidiplomasia kukabiliana na tishio kubwa la ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ametahadharisha kuwa, kuibuka tena ugaidi nchini Syria na kuenea kwake katika eneo kutaleta tishio kubwa kwa amani, utulivu na usalama na hivyo ametaka kuwepo juhudi kukabiliana na tishio hilo.

Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty, siku ya Jumatano, Araghchi alisema ni muhimu kukabiliana na tishio kubwa la ugaidi kupitia juhudi za kidiplomasia na mashauriano kati ya nchi zenye ushawishi mkubwa wa kikanda.

Magaidi wanaoungwa mkono na madola ya kigeni wakiongozwa na kundi la Takfiri la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) walianzisha mashambulizi makubwa katika majimbo ya Aleppo na Idlib kaskazini-magharibi mwa Syria mnamo Novemba 27, wakiteka maeneo kadhaa.

Tangu wakati huo, vikosi vya serikali ya Syria vimekuwa vikikabiliana vikali na magaidi hao ili kurejesha ardhi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua juu ya matokeo ya mazungumzo yake na maafisa wakuu wa Syria na Uturuki wakati wa ziara yake huko Damascus na Ankara, na kusisitiza msimamo thabiti wa Tehran wa kuunga mkono serikali, jeshi na taifa la Syria katika mapambano dhidi ya vikundi vya kigaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, kwa upande wake, amesema amefanya mazungumzo ya simu na baadhi ya mawaziri wenzake katika siku za hivi karibuni na kusisitiza kwamba sera ya Misri ni kuunga mkono serikali ya Syria.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Misri pia walikubaliana kufanya mawasiliano zaidi kuhusu matukio ya kieneo.