Kampuni ya Ufaransa yapoteza udhibiti wa mgodi mkubwa wa urani nchini Niger
Kampuni ya fueli nyuklia ya Ufaransa iitwayo Orano imesema kuwa, serikali ya Niger imechukua udhibiti wa mgodi wa urani wa Somair uliokuwa umehodhiwa na shirika hilo la kikoloni katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kampuni ya kikoloni ya Orano ambayo ilikuwa inamiliki takriban asilimia 63 ya mgodi huo imesema katika taarifa yake kwamba maamuzi yaliyochukuliwa katika vikao vya bodi ya Somair hayana itibari tena.
Serikali ya Niger inasema kuwa, wananchi wa nchi hiyo ndio wenye haki ya kunufaika na maliasili za nchi yao zikiwemo za mgodi muhimu sana wa Sonar unaozalisha madini ya urani. Kampuni ya Orano ya mkoloni kizee Ufaransa ilifutiwa kibali muhimu cha uchimbaji madini mwezi Juni 2024. Baada ya hapo ilipigwa marufuku kusafirisha madini nje ya Niger.
Lakini kampuni hiyo ya kikoloni iliendelea kung'ang'ani kubakia Niger licha ya kukumbwa na matatizo ya kifedha tangu wakati huo hadi hivi sasa ambapo imethibitisha kuwa imepoteza kikamilifu udhibiti wa mgodi huo.
Kwa muda mrefu sana Ufaransa imekuwa ikinyonya utajiri wa maliasili wa nchi za Afrika ikiwemo Niger, huku wananchi wa nchi hizo wakiendelea kuteseka kwa mabalaa na matatizo chungu nzima. Utawala mpya uliongia madarakani nchini Niger umeamua kukomesha dhulma na unyonyaji wa dola hilo la kikoloni la Ulaya.
Madini ya urani yanatumika sana katika nishati ya nyuklia. Kampuni ya Orano ya mkoloni Ufaransa imekuwa ikikomba utajiri wa madini wa Niger kwa miaka mingi.
Serikali ya Niger imesema kuwa ina mpango wa kufanyia marekebisho sheria ili kulinda rasilimali za nchi hiyo.