DRC: Idadi ya vifo vya ugonjwa usiojulikana yafikia 143
Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa ajabu usiojulikana katika jimbo la kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeongezeka na kufikia 143. Idadi ya vifo imeendelea kuongezeka huku waziri wa afya akitangaza kwamba timu ya wataalamu imetumwa ili kubaini asili halisi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo, serikali ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Desemba 4 kwamba ugonjwa huu umesababisha vifo vya watu 79.
Serikali ya DRC inabainisha kuwa waathiriwa wengi ni watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 15. Hadi sasa, watu 376 wameathiriwa na ugonjwa huu ambao bado haujajulikana.
Ni tangu Jumapili, Novemba 10 ambapo vifo vya kwanza viliripotiwa katika eneo la afya la Panzi, katika eneo la Kasongo-Lunda.
Waziri wa Afya Samuel Kamba Roger alisema katika taarifa iliyotolewa Jumatano kwamba dalili za ugonjwa huo zinaweza kuashiria magonjwa kadhaa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na mpox na Ebola, ambayo yote yamesababisha wasiwasi mkubwa nchini DR Congo.
Aliongeza kuwa serikali imetuma timu ya wataalam wa magonjwa ya milipuko ili kutathmini hali na kujua asili ya ugonjwa huo.
Amethibitisha kuwa mlipuko huu tayari umesababisha vifo vya watu 79, jambo ambalo limeitia hofu serikali ya mkoa wa Kwango.