Umoja wa Mataifa wazidisha juhudi za kufufua mchakato wa kisiasa Libya
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umesema kwamba umeongeza jitihada zake za kufufua mchakato wa kisiasa na kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kitaifa nchini humo.
Taarifa ya timu hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema: "Katika siku chache zilizopita, Stephanie Koury, afisa-msimamizi wa UNSMIL, amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa wakuu wa Libya na kujadiliana nao suala hilo."
Koury amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge lenye makao yake mashariki (HoR), Aguila Saleh, Rais wa Baraza la Uongozi Mohamed al-Menfi, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje, Taher Al-Baour, na Waziri wa Nchi wa Masuala ya Kisiasa na Mawasiliano, Walid Ellafi.
Mazungumzo hayo yamehusu kuunganishwa taasisi za serikali, hasa taasisi za utendaji, kuwezesha uchaguzi wa kuaminika na kuanzishwa bajeti ya pamoja kwa ajili ya mwaka ujao.
Walijadiliana pia haja ya kuvunjwa mkwamo uliopo hivi sasa wa kisiasa na kuandaliwa mazingira mazuri ya uchaguzi "kwa misingi ya kisheria na kisiasa."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Koury amewataka viongozi hao waongeze juhudi za kukomeshwa tabia ya kuchukuliwa hatua za upande mmoja ambazo zinazidisha mgawanyiko wa kitaasisi nchini Libya.
Libya imetumbukia kwenye misukosuko ya kisiasa tangu ulipoangushwa utawala wa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi mwaka 2011. Nchi hiyo sasa imegawanyika kati ya tawala mbili hasimu yaani serikali yenye makao yake mashariki mwa nchi, na serikali yenye makao yake katika mji mkuu Tripoli huko magharibi mwa Libya.