Umoja wa Mataifa: Sudan inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu
Kwa mara nyingine tena Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa na itakayoendelea kushuhudiwa nchini Sudan.
Onyo hilo la Umoja wa Mataifa linatolewa wakati huu ambapo tayari hali ya njaa ikiwa imetangazwa kwenye taifa hilo.
Mwezi Juni, kamati maalumu ya umoja wa Mataifa inayofuatilia mwenendo wa upatikanaji wa chakula duniani, ilisema watu zaidi ya laki 7 nchini humo wanakabiliwa na baa la njaa na kwamba kunahitajika udharura wa kushughulikia mzozo unaoendelea.
Tayari mashirika kadhaa ya kibinadamu ya umoja wa Mataifa na yale washirika, wametangaza njaa kwenye kambi kubwa zaidi ya wakimbizi ya Zamzam, ambako wapiganaji wa RSF wanaendeleza mashambulio.
Juma lililopita, umoja wa mataifa kupitia ofisi yake ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, ulisema licha ya kufanikiwa kufikisha misaada katika baadhi ya maeneo ambako raia wanahitaji msaada wa dharura, lakini kulihitajika juhudi za ziada kuwafikia watu mamilioni ya raia ambao wanaendelea kukimbia machafuko.
Mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya zaidi kwani karibu watu milioni 6.8 wamekimbia makazi yao kutafuta usalama nchini Sudan au nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa hadi sasa zimeshindwa kukomesha mapigano hayo.