Tanzania na Imarati zaazimia kuboresha uhusiano baina yao
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zimesisitiza kuwa, zina azma ya kuimarisha ushirikiano baina yao katika nyanja mbalimbali.
Sisitizo hilo limetolewa katika Kikao cha Kwanza cha Mashauriano ya Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE mjini Abu Dhabi.
Kupitia mazungumzo hayo ya kwanza na ya aina yake, Tanzania na Imarati zimehakikishiana dhamira zao za kuendelea kushirikiana kwa karibu kuboresha uhusiano uliopo ili kuufikisha katika viwango vya juu kwa manufaa ya nchi na wananchi wa pande zote mbili.
Aidha, Tanzania na Imarati zimeongelea pia umuhimu wa kushirikiana kiuchumi na kuwa na ushirikiano wa kina uliojengwa juu ya msingi wa kuaminiana, ambao umeyafanya mataifa haya kushirikiana kwa karibu katika kushughulikia masuala mbalimbali ya pande mbili na ya kimataifa kwa maslahi ya pamoja.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho.