Mlipuko wa kipindupindu nchini Sudan Kusini 'unaongezeka kwa kasi'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119826-mlipuko_wa_kipindupindu_nchini_sudan_kusini_'unaongezeka_kwa_kasi'
Shirika moja la misaada ya kibinadamu limeonya kuwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Sudan Kusini "unaongezeka kwa kasi",  ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya kesi ya kwanza kugunduliwa.
(last modified 2024-12-07T03:42:31+00:00 )
Dec 07, 2024 03:42 UTC
  • Mlipuko wa kipindupindu nchini Sudan Kusini 'unaongezeka kwa kasi'

Shirika moja la misaada ya kibinadamu limeonya kuwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Sudan Kusini "unaongezeka kwa kasi",  ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya kesi ya kwanza kugunduliwa.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, linalojulikana kwa kifupi cha Kifaransa MSF, lilisema Ijumaa kuwa jumla ya visa 737 vya kipindupindu vimeripotiwa huko Malakal, mji mkuu wa jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Katika taarifa ya Ijumaa, MSF ilisema kuwa timu zake zimeanzisha kituo cha matibabu ya kipindupindu chenye vitanda 100 karibu na Hospitali ya Mji wa Malakal, lakini changamoto kubwa ni katika upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira.

Kufikia Desemba 3, Sudan Kusini ilikuwa imeripoti kesi 1,526 za ugonjwa huo ambao husabaishwa na kutozingatia usafi wa kimazingira.

Kipindupindu husababishwa na vijidudu ambavyo kwa kawaida husambazwa kwa kukosa huduma ya usafi wa mazingira. Watu huambukizwa wanapokula chakula au kunywa maji yanayobeba vijidudu hivyo.