Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inapambana na ugonjwa usiojulikana
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, iko kwenye tahadhari ya hali ya juu kutokana na ugonjwa usiofahamika ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 140 katika kipindi cha mwezi mmoja.
Samuel Roger Kamba, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasiia ya Congo, amesema kuwa, wizara yake iko katika hali ya tahadhari na kwamba wanachukulia tukio hilo kama kiwango cha janga linalohitaji kufuatiliwa.
Serikali ya DRC inabainisha kuwa waathiriwa wengi ni watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 15. Hadi sasa, watu 376 wameathiriwa na ugonjwa huu ambao bado haujajulikana.
Ni tangu Jumapili, Novemba 10 ambapo vifo vya kwanza viliripotiwa katika eneo la afya la Panzi, katika eneo la Kasongo-Lunda.
Waziri wa Afya Samuel Kamba Roger aenuukuliiwa akisema kwamba dalili za ugonjwa huo zinaweza kuashiria magonjwa kadhaa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na mpox na Ebola, ambayo yote yamesababisha wasiwasi mkubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Aliongeza kuwa serikali imetuma timu ya wataalam wa magonjwa ya milipuko ili kutathmini hali na kujua asili ya ugonjwa huo.