Msumbiji yaendelea kukumbwa na maandamano baada ya uchaguzi; watu 20 wajeruhiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119858-msumbiji_yaendelea_kukumbwa_na_maandamano_baada_ya_uchaguzi_watu_20_wajeruhiwa
Takriban watu 20 jana walijeruhiwa katika makabiliano na polisi ya Msumbiji katika maandamano makubwa yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo kupinga uchaguzi wa rais wa tarehe 9 Oktoba. Aidha majengo mawili ya serikali katika mji mkuu Maputo yalichomwa moto na waandamanaji wenye silaha.
(last modified 2024-12-07T23:27:01+00:00 )
Dec 07, 2024 23:27 UTC
  • Msumbiji yaendelea kukumbwa na maandamano baada ya uchaguzi; watu 20 wajeruhiwa

Takriban watu 20 jana walijeruhiwa katika makabiliano na polisi ya Msumbiji katika maandamano makubwa yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo kupinga uchaguzi wa rais wa tarehe 9 Oktoba. Aidha majengo mawili ya serikali katika mji mkuu Maputo yalichomwa moto na waandamanaji wenye silaha.

Mgombea wa kiti cha urais wa upinzani, Venancio Mondlane ametoa wito akiwataka wafuasi wake kuandamana kwa wiki nzima ikiwa ni katika marhala mpya ya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais huko Msumbiji. 

Venancio Mondlane

Orlando Mudumane Msemaji wa Polisi ya Taifa ya Msumbiji ameviambia vyombo vya habari kuwa waandamanaji waliweka vizuizi katika barabara za mji mkuu Maputo huku wakichoma matairi na kurusha mawe. 

Amesema, waandamanaji walitumia mabomu yanayotengenezwa nyumbani kulipua majengo mawili ya serikali. 

Katika maandamano ya jana Msumbiji, watu 20 wamejeruhiwa katika makabiliano na polisi ambao piai walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Maandamano yalianza nchini Msumbiji Oktoba 24 mwaka huu baada ya tUme ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo kumtangaza mgombea wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) Daniel Chapo kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais kuibuka na ushindi wa asilimia 70 ya kura zilizopigwa, huku Mondlane akishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 20, jambo lililompelekea kupinga matokeo ya uchaguzi na kutoa wito kwa wananchi kuandamana kulalamikia matokeo ya uchaguzi. 

Takriban watu 90 wameuawa na wengine 340 kujeruhiwa tangu ghasia za baada ya uchaguzi kuikumba Msumbiji mwezi Oktoba mwaka huu.