Naibu Rais wa Kenya atekeleza sera tofauti na mtangulizi wake
-
Prof Kithure Kindiki
Naibu wa Rais wa Kenya, Prof Kithure Kindiki anaonekana kuchukua hatua za kimakusudi kuepuka makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake, Rigathi Gachagua, kwa kukwepa hafla za umma zinazohudhuriwa na Rais William Ruto tangu aapishwe kuwa naibu wa rais wa tatu wa Kenya.
Ripoti zinasema, tofauti na mtangulizi wake aliyeonekana katika takriban hafla zote za Rais, Prof Kindiki anaonekana kufuata mwelekeo tofauti wa kuepuka mienendo iliyochangia naibu wa pili wa Rais wa Kenya kutimuliwa madarakani.
Wachanganuzi wa siasa wanahusisha mtindo wa Prof Kindiki na weledi wa kutojisawiri kama rais mdogo alivyokuwa akifanya Gachagua.
Akizungumzia mienendo ya Prof Kithure Kindiki katika nafasi yake ya sasa kama Naibu Rais wa Kenya, mdadisi wa siasa Paul Wafula anasema: “Ni weledi na hekima ambayo imemfanya kuwa na ratiba yake tofauti na Rais na kuepuka makosa yaliyofanywa na Gachagua aliyejitokeza kama mwenza wa Ruto serikalini.”
Wafula anasema: Tofauti na Gachagua, Prof Kindiki amekuwa mstari wa mbele kupigia debe miradi ya serikali katika hafla zake.
Oktoba mwaka huu Baraza la Seneti nchini Kenya liliidhinisha uamuzi wa kumuondoa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua kutokana na mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake, katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Gachagua alikabiliwa na msururu wa tuhuma zikiwemo za ufisadi, kukiuka katiba, kumhujumu rais na kushajiisha migawanyiko ya kikabila.
Gachagua amekuwa Naibu Rais wa kwanza kuvuliwa mamlaka na Bunge chini ya Katiba ya 2010.