Knut yaitaka TSC iajiri washauri kuzuia visa vya walimu kujitia kitanzi Kenya
Chama cha Walimu Kenya (KNUT) kimeitaka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iajiri washauri nasaha kushughulikia visa vya kujitia kitanzi na matumizi mabaya dawa za kulevya kwa walimu nchini humo.
TSC inasema walimu wengi wanasumbuliwa na magonjwa ya akili, hali ambayo imeathiri utendakazi wao na kusambaratisha familia zao.
Mwakilishi wa Kike wa Kwanza wa Kitaifa, Mercy Ndung’u amesema maelfu ya walimu wanaumia lakini wao huwa wananyamaza tu.
“Walimu wanahitaji huduma za ushauri popote walipo nchini. Ni huduma ya lazima ambayo inafaa kutolewa na wizara na mwaajiri ili kuokoa maisha,” amesema Bi Ndung’u katika hafla ya kuadhimisha siku 16 za kukabili dhuluma za kijinsia mjini Bomet mwisho wa juma.
Aamesema: “Baadhi ya changamoto za walimu huwasababisha kujihusisha na utumiaji mbaya wa dawa za kulevya ili waepuke hali halisi ya maisha. Ni suala ambalo linafaa kuangaziwa na washikadau wote wa elimu nchini.”
Mwakilishi mwanamke wa KNUT tawi la Bomet, Betty Langat amesema baadhi ya walimu wamejiua kwa sababu ya msongo wa mawazo, huku baadhi wakianza uraibu wa pombe baada ya kukosa msaada wa kisaikolojia.
Tukio la hivi karibuni zaidi la kujitia kitanzi ni la mwalimu wa shule ya upili ya Kenya High jijini Nairobi.
Mwili wa mwalimu huyo ulipatikana ukining’inia katika ngazi ya tenki ya maji shuleni hapo tarehe Pili Oktoba 2024.