Wapinzani Burundi wakosoa sheria mpya za uchaguzi wa Bunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119942-wapinzani_burundi_wakosoa_sheria_mpya_za_uchaguzi_wa_bunge
Mrengo wa upinzani nchini Burundi umekosoa vikali maagizo ya Rais Evariste Ndayishimiye kuhusu uchaguzi wa Bunge ambao umepangwa kufanyika Juni 5 mwaka ujao, wakisema yanalenga kumzuia aliyekuwa kiongozi wa chama cha CNL Agathon Rwasa kugombea katika uchaguzi huo.
(last modified 2024-12-09T23:20:09+00:00 )
Dec 09, 2024 23:20 UTC
  • Wapinzani Burundi wakosoa sheria mpya za uchaguzi wa Bunge

Mrengo wa upinzani nchini Burundi umekosoa vikali maagizo ya Rais Evariste Ndayishimiye kuhusu uchaguzi wa Bunge ambao umepangwa kufanyika Juni 5 mwaka ujao, wakisema yanalenga kumzuia aliyekuwa kiongozi wa chama cha CNL Agathon Rwasa kugombea katika uchaguzi huo.

Rais Evariste Ndayishimiye, akithibitisha kuandaliwa uchaguzi huo mwaka ujao, ametangaza kanuni za uchaguzi ambazo zinawazuia viongozi wa vyama kuwania kwenye uchaguzi huo au wawe wamejiuzulu au kufurushwa kwenye uongozi kwa muda wa miaka miwili.

Maagizo hayo ya Rais wa Burundi yanasisitiza wagombea huru wataruhusiwa kuwania iwapo hawajakuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa kwa muda wa mwaka moja.

Masharti hayo sasa yamepingwa na wapinzani wanaosema yameundwa kumzuia moja kwa moja kinara wa chama cha CNL aliyeondolewa, Agathon Rwasa.

Chama cha CNL kilipigwa marufuku mwezi Agosti na Wizara ya Usalama wa Ndani kufuatia mikutano miwili ya baraza kuu, moja ya mkutano huo ukiwa umesababisha kuondolewa madarakani Agathon Rwasa.

Burundi imekuwa ikituhumiwa kwamba, inakiuka haki za binadamu. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema katika ripoti yake Agosti mwaka huu kwamba, Burundi imeshuhudia vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais wa nchi hiyo, Evariste Ndayishimiye.