Magenge ya kigaidi yaua raia 21 nchini Niger
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119950-magenge_ya_kigaidi_yaua_raia_21_nchini_niger
Raia 21 waliuawa wiki iliyopita wakati magaidi waliposhambulia msafara wa usafirishaji wa bidhaa karibu na Tera, magharibi mwa Niger. Hilo ni eneo ambalo mara kwa mara hushambuliwa na watu wasiojulikana wenye silaha.
(last modified 2024-12-10T03:01:51+00:00 )
Dec 10, 2024 03:01 UTC
  • Magenge ya kigaidi yaua raia 21 nchini Niger

Raia 21 waliuawa wiki iliyopita wakati magaidi waliposhambulia msafara wa usafirishaji wa bidhaa karibu na Tera, magharibi mwa Niger. Hilo ni eneo ambalo mara kwa mara hushambuliwa na watu wasiojulikana wenye silaha.

Redio ya serikali ya Niger inayoitwa Voix du Sahel imethibitisha kuwa shambulio hilo lilitokea kwenye eneo la pembe tatu linalozikutanisha nchi za Niger, Mali na Burkina Faso.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana imesema: "Magari yaliyokuwa yakirudi kutoka kwenye soko la kila wiki huko Tera yalishambuliwa na majambazi wenye silaha Disemba 5, katika eneo lililoko umbali wa kilomita 12 kaskazini mwa Tera, karibu na Bankilare."

Jeshi la Niger linaendelea na operesheni kadhaa za kupambana na magenge ya kigaidi katika eneo la Tillaberi, ambako kunatokea mashambulizi ya mara kwa mara magaidi.

Hali ya kiusalama imezidi kuwa changamoto kwa Niger baada ya serikali ya nchi hiyo kuamua maliasili za nchi zimilikiwe na ziwanufaishe wananchi wenyewe na si madola ya kikoloni ya Ulaya.

Niger imeyatimua mashirika ya kinyonyaji wa madola ya kikoloni ya Magharibi hasa Ufaransa ikiwemo kampuni ya fueli nyuklia ya Ufaransa iitwayo Orano ambayo hivi karibuni ililalamika kuwa, serikali ya Niger imechukua udhibiti wa mgodi wa urani wa Somair uliokuwa umehodhiwa na shirika hilo la kikoloni katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kwa muda mrefu sana Ufaransa imekuwa ikinyonya utajiri wa maliasili wa nchi za Afrika ikiwemo Niger, huku wananchi wa nchi hizo wakiendelea kuteseka kwa mabalaa na matatizo chungu nzima. Utawala mpya uliongia madarakani nchini Niger umeamua kukomesha dhulma na unyonyaji wa dola hilo la kikoloni la Ulaya.