Polisi Kenya watawanya maandamano ya wapinzani wa ukatili dhidi ya wanawake
Polisi nchini Kenya wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kutawanya waandamanaji wanaopinga ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake nchini humo.
Waandamanaji hao waliokuwa wakipiga nara za "Komesha Mauaji ya Wanawake", walitawanywa na polisi katika bustani ya umma ambapo walikuwa wamekusanyika baadaye kushiriki katika mapigano barabarani. Waandamanaji kadhaa wamejeruhiwa katika makabiliano hayo ya leo Jumanne.
“Inasikitisha sana kwamba nimejeruhiwa nikipinga suala la wanawake kujeruhiwa au kuuawa. Ikiwa rais ana nia ya dhati ya kukomesha mauaji ya wanawake, aanze kwa kuwachukulia hatua maafisa ambao wametufanyia unyama leo,” amesema mwanaharakati Mwikali Mueni.
Takribani watu watatu wamekamatwa, huku waandaaji wakisema polisi walikataa ombi lao la kufanya maandamano.
Kenya inasumbuliwa na janga la kimya kimya la unyanyasaji wa kijinsia. Mwezi Oktoba Polisi walisema wanawake 97 wameuawa tangu Agosti, wengi wao wakiuawa na wapenzi wao kiume.
Mwezi uliopita, Rais William Ruto alisema serikali yake imejitolea kushughulikia matukio hayo yanayoongezeka, na aliahidi dola 800,000 kwenye kampeni iliyopewa jina la "Nyumba Salama, Nafasi Salama".
Waandamanaji hao wanatoa wito wa kukomeshwa ongezeko la unyanyasaji dhidi ya wanawake, na kuchukuliwa sheria kali zaidi za kuwashtaki wahalifu.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi Novemba ya kuanza kampeni tofauti ya siku 16 duniani ilisema Afrika imerekodi kiwango cha juu zaidi cha mauaji ya wanawake yanayohusiana na washirika mnamo 2023.
Leo ni siku ya mwisho ya siku 16 za wanaharakati kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.