Wachimba migodi 10 wanahofiwa kufariki dunia katika mgodi wa dhahabu Kenya
Watu kumi wanahofiwa kufariki baada ya machimbo ya dhahabu ya kuporomoka huko Dabel kaunti ya Marsabit mashariki mwa Kenya.
Licha ya kufungwa migodi hiyo Machi mwaka huu baada ya watu 13 kufariki dunia kufuatia mgongano wa jinsi ya kugawana rasilimali hiyo, uchimbaji umeendelea kinyume cha sheria kwa msaada wa baadhi ya maofisa wa usalama.
Chifu wa eneo hilo la Dabel Ibrahim Dube alithibitisha Jumatano kuwa miili saba ilitolewa kutoka mgodi huo ulioporomoka Jumanne, na kuongeza kuwa kazi ya uokoaji inaendelea.
Wakazi wa eneo hilo wanasema kulikuwa na wachimbaji 10 walioingia kinyemela katika eneo lililozuiliwa kuendelea na uchimbaji. Kwa msingi huo kuna hofu kuwa watu wote 10 waliokuwemo wamepoteza maisha.
Kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau hakuthibitisha idadi ya watu waliopoteza maisha akisema hakuwa na taarifa za moja kwa moja.
Akizungumza alipozuru Moyale mnamo Desemba 3, 2024, Katibu Mkuu wa Idara ya Madini Kenya Elijah Mwangi alisema uchimbaji madini utafunguliwa baada ya serikali kukamilisha utekelezaji wa sheria ya uchimbaji madini.
Kabla ya kufungwa, migodi ya Hillo ilivutia karibu watu 70,000 huku takriban asilimia 80 ya watu wakijumuisha wahamiaji haramu kutoka Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tanzania, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na Nigeria wakishiriki.