ECOWAS kutumia diplomasia kuzishawishi Burkina Faso, Mali na Niger kurejea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120036-ecowas_kutumia_diplomasia_kuzishawishi_burkina_faso_mali_na_niger_kurejea
Rais Bola Tinubu wa Nigeria amesema kuwa, maslahi na ustawi wa raia wa Burkina Faso, Mali na Niger utaendelea kuwa kipaumbele kwa viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) yenye wanachama 15, na amesisitiza kuwa, jumuiya hiyo itatumia diplomasia na hekima kuhakikisha nchi hizo tatu zinarejea katika jumuiya hiyo ya kikanda.
(last modified 2024-12-12T02:57:44+00:00 )
Dec 12, 2024 02:57 UTC
  • ECOWAS kutumia diplomasia kuzishawishi Burkina Faso, Mali na Niger kurejea

Rais Bola Tinubu wa Nigeria amesema kuwa, maslahi na ustawi wa raia wa Burkina Faso, Mali na Niger utaendelea kuwa kipaumbele kwa viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) yenye wanachama 15, na amesisitiza kuwa, jumuiya hiyo itatumia diplomasia na hekima kuhakikisha nchi hizo tatu zinarejea katika jumuiya hiyo ya kikanda.

Akimpokea Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria jana Jumatano, Tinubu, ambaye ni mwenyekiti wa hivi sasa wa ECOWAS amesema kuwa, viongozi wa nchi hizo tatu hadi sasa wameendelea kukataa kupeleka mipango yao ya kurejea katika jumuiya hiyo.

Rais Tinubu amesema: "Uhusiano wetu wa kuheshimiana utaendelea iwapo tutatathmini upya hali ya hivi sasa katika nchi hizo tatu. Ninachoweza kuhakikisha ni kwamba hatuwezi kuzivumilia serikali zisizo za kikatiba... Tuna raia wasio na hatia ambao ni wahanga wa mapinduzi ya kijeshi. Tutaendelea kuchunguza njia za kidiplomasia bila ya kuwaadhibu wananchi wasio na hatia."

Tarehe 28 Januari 28, 2024, Burkina Faso, Mali na Niger kwa pamoja zilitangaza kujiondoa katika jumuiya ya ECOWAS ikiwa ni kujibu vikwazo vilivyowekwa na jumuiya hiyo dhidi ya nchi hizo tatu. Hatua hiyo iliitikisa jumuiya ya kikanda ya ECOWAS ambayo ililegeza kamba na kuondoa vikwazo hivyo, lakini hadi leo nchi hizo tatu hazijarejea.

Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa, ziara ya Rais wa Ujerumani nchini humo imefanyika ili kuimarisha ushirikiano hasa wa nishati kati ya nchi hizo mbili.