Wasimamiaji wa usitishaji vita wanahofia kuzorota usalama Sudan Kusini
Wasimamiaji wa makubaliano ya usitishaji vita Sudan Kusini wamesema kwamba, wamepata wasiwasi mkubwa wa kuzorota hali ya usalama katika Kaunti ya Tambura ya Jimbo la Equatoria Magharibi, huko kusini-magharibi mwa Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.
Yitayal Gelaw Bitew, mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Usitishaji Vita nchini Sudan Kusini amesema kuwa, hali ya usalama katika Kaunti ya Tambura imeendelea kutia wasiwasi baada ya kutokea jaribio la mauaji ya kamishna wa kaunti tarehe 28 mwezi uliopita wa Novemba 2024.
Taarifa zinasema kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, watu wenye silaha walishambulia makazi ya Kamishna wa Kata ya Tambura, Matthew Mabenge kwa roketi na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha.
Gelaw amesema: "Shambulio hilo lilikuwa ni jaribio la pamoja la kumwondoa mkuu huyo ofisini na kudhoofisha amani na usalama katika Kaunti ya Equatoria Magharibi."
Mapigano ya kikabila yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye Kaunti ya Tambura tangu mwezi Juni 2021 na yamepelekea Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini kuingilia kati.
Tarehe 8 Novemba 2024, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) uliimarisha doria za kulinda amani baada ya kutolewa ripoti za kuhamasishwa makundi yenye silaha yafanye mashambulizi katika maeneo tofauti. Hali hiyo imeongeza mvutano na hofu miongoni mwa jamii za wenyeji wa Kaunti ya Tambura.
Ujumbe huo wa kulinda amani pia umesema kuwa, idadi ya watu waliokimbia makazi yao na kutafuta hifadhi karibu na kambi ya muda ya UNMISS ya Tambura imeongezeka kutoka karibu 3,700 hadi zaidi ya 10,500.