Afrika Kusini yafungua tena kivuko cha mpakani na Msumbiji
Mamlaka ya Kusimamia Mipaka ya Afrika Kusini (BMA) imetangaza kuwa, harakati za wasafiri katika kivuko kikuu cha mpaka wa Afrika Kusini na Msumbiji sasa ziko wazi hadi litakapotolewa tangazo jingine.
Hatua hiyo imekuja baada ya BMA kusimamisha kwa muda shughuli katika kivuko cha Lebombo siku ya Jumatatu kutokana na maandamano yanayohusiana na uchaguzi nchini Msumbiji yaliyotokea karibu na eneo la mpakani. Maandamano haya yamelazimisha kufungwa mara kwa mara kivuko hicho tangu yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Msumbiji tarehe 24 Oktoba mwaka huu wa 2024.
Chama cha Usafirishaji Mizigo cha Afrika Kusini (RFA) kilisema Jumanne kwamba kusimamishwa shughuli za kivuko cha Lebombo kunasababisha hasara ya takriban randi milioni 10 (kama dola za 562,400 za Kimarekani) kila siku.
Kabla ya hapo vyombo vya habari vilikuwa vimeripoti kuwa, waandamanaji upande wa Msumbiji wamefunga njia muhimu ambayo kwa kawaida hutumiwa na zaidi ya malori 1,000 yanayosafiri kila siku kuelekea Bandari ya Maputo. Kufungwa kwa muda njia hiyo kunasababisha kukatika huduma na kuchelewa kufika bidhaa na abiria. Hivi sasa kunashuhudiwa msururu mrefu wa malori yanayosubiri kuingia Msumbiji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati ya Bunge la Afrika Kusini imemaliza ziara yake ya kukagua eneo hilo na kubainisha wasiwasi wake kuhusu athari za kuchelewa kwa muda mrefu uvuushaji bidhaa mpakani kutokana na maandamano ya nchini Msumbiji.
Katika tamko lake, kamati hiyo ya Bunge la Afrika Kusini imesema: "Ushirikiano endelevu ni muhimu kati ya serikali ya Afrika Kusini na Msumbiji ili kupata masuluhisho ya changamoto za hivi sasa."