Wagombea wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika washiriki katika mjadala
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120140-wagombea_wa_uenyekiti_wa_tume_ya_umoja_wa_afrika_washiriki_katika_mjadala
Wanasiasa watatu wa Kiafrika wanaotaka kuongoza Tume ya Umoja wa Afrika Ijumaa walishiriki katika mjadala ambapo walieleza kwa kina mipango yao kwa ajili ya usalama wa kikanda huku wakitetea vikali biashara baina ya nchi Afrika miongoni mwa masuala mengine.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 14, 2024 08:57 UTC
  • Wagombea wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika washiriki katika mjadala

Wanasiasa watatu wa Kiafrika wanaotaka kuongoza Tume ya Umoja wa Afrika Ijumaa walishiriki katika mjadala ambapo walieleza kwa kina mipango yao kwa ajili ya usalama wa kikanda huku wakitetea vikali biashara baina ya nchi Afrika miongoni mwa masuala mengine.

Raila Odinga wa Kenya, Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar wanatafuta kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja.

Watatu hao walishiriki katika mjadala wa saa mbili katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa ambapo wote walitetea viti viwili vya kudumu kwa nchi za Kiafrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Odinga alisema kuwa viti viwili vya kudumu vilivyo na mamlaka ya kura ya turufu ni "lazima kwa Afrika" na kwamba viti hivyo ni haki isiyopingika kwani bara hilo lina zaidi ya nchi 50.

Randriamandrato alizitaka nchi wanachama "kuzungumza kwa sauti moja juu ya chaguo la nani atawakilisha Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Youssouf alisema kuwa usalama wa kikanda unaweza kuimarishwa ikiwa rasilimali za kikosi kijeshi cha Umoja wa Afrika zitaongezwa ili kupunguza utegemezi mkubwa kwa madola ya kigeni.

Hivi sasa idadi ya watu barani Afrika ni bilioni 1.3 na idadi ya vijana barani humo inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050. Pamoja na hayo lakini biashara ya kikanda imekabiliwa na changamoto na hiyo ilikuw amoja ya mada zilizoshughulikiwa katika mjadala wa Ijumaa.

Watatu hao wanajaribu kuzishawishi nchi nyingi za Afrika kabla ya uchaguzi wa Februari kumrithi Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki, ambaye amehudumu kwa mihula miwili.