42 wauawa katika mripuko wa bomu la ardhini katikati mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120148-42_wauawa_katika_mripuko_wa_bomu_la_ardhini_katikati_mwa_sudan
Takriban watu 42 wameuawa katika mripuko wa bomu la kutegwa ardhini kwenye Jimbo la Sinnar la katikati mwa Sudan. Vikundi vya kujitolea vinakituhumu Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kuhusika na shambulio hilo.
(last modified 2024-12-14T23:35:09+00:00 )
Dec 14, 2024 23:35 UTC
  • 42 wauawa katika mripuko wa bomu la ardhini katikati mwa Sudan

Takriban watu 42 wameuawa katika mripuko wa bomu la kutegwa ardhini kwenye Jimbo la Sinnar la katikati mwa Sudan. Vikundi vya kujitolea vinakituhumu Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kuhusika na shambulio hilo.

Kikundi kimoja cha kujitolea cha mji wa Al-Suki wa Jimbo la Sennar, kimetoa taarifa na kusema kuwa, watu 13 wameuawa katika eneo la Al-Suki na wengine wengi kujeruhiwa wakati bomu la ardhini liliporipuka kwenye lori lao.

Tarehe 5 Oktoba mwaka huu, Jeshi la Sudan (SAF) lilitangaza kuwa limelichukua tena eneo la kimkakati la Jebel Moya huko Sinnar ambalo liko kwenye njia panda inayounganisha majimbo ya Gezira, White Nile na Sinnar. Kutekwa tena eneo la Jebel Moya kuliliwezesha jeshi la Sudan (SAF) kuwazingira wapiganaji wa RSF huko Sinnar na kukata njia zao za mawasiliano na usambazaji wa vifaa vya kilojistiki. 

Vikundi hivyo vya kujitolea vimesema kuwa, raia 29 waliuawa kwenye siku za Jumatano na Alkhamisi katika mashambulizi ya RSF kwenye vijiji kadhaa vya Jimbo la Gezira.

Kikundi kingine cha kujitolea cha Nidaa Al-Wasat Platform kimeripoti kwamba vikosi vya RSF vyenye silaha vilivyokuwa juu ya pikipiki na magari ya kivita, vilishambulia vijiji kadhaa vya maeneo ya Al-Huda na Al-Managil huko Gezira siku ya Jumatano na kuua watu 24 na kuwajeruhi wengine wapatao 30.

Hata hivyo hadi wakati tunaandaa taarifa hii, Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vilikuwa havijasema chochote kuhusu taarifa hizo.