Vikosi vya Tunisia vyasambaratisha mtandao mwingine wa mihadarati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120190-vikosi_vya_tunisia_vyasambaratisha_mtandao_mwingine_wa_mihadarati
Kituo cha redio cha Mosaique FM kimeripoti kuwa, vikosi vya usalama vya Tunisia vimesambaratisha mtandao mwingine dawa za kulevya katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Ariana, na kuwatia mbaroni watu wanne raia wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
(last modified 2024-12-15T23:08:23+00:00 )
Dec 15, 2024 23:08 UTC
  • Vikosi vya Tunisia vyasambaratisha mtandao mwingine wa mihadarati

Kituo cha redio cha Mosaique FM kimeripoti kuwa, vikosi vya usalama vya Tunisia vimesambaratisha mtandao mwingine dawa za kulevya katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Ariana, na kuwatia mbaroni watu wanne raia wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Operesheni hiyo ilianza kwa kukamatwa mshukiwa mmoja aliyekuwa amebeba dawa za kulevya aina ya kokeini na kusababisha kuvamiwa nyumba yake ambapo watu wengine watatu akiwemo mwanamke mmoja walikamatwa.

Operesheni iliyopelekea kukamatwa idadi kubwa ya madawa ya kulevya aina ya kokeini na bangi ilifanyika siku ya Jumamosi, imesema taarifa hiyo lakini haitoa maelezo zaidi wala uraia wa watu waliotiwa mbaroni. 

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba pia, vikosi vya usalama vya Tunisia vilisambaratisha mitandao miwili ya magendo ya dawa za kulevya katika majimbo ya Ben Arous na Ariana karibu na mji mkuu, Tunis.

Radio ya Taifa ya Tunisia iliripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, vitengo vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kusambaratisha magenge hayo katika operesheni mbili tofauti na kuwatia mbaroni watu tisa na kukamata kiasi kisichojulikana cha dawa za kulevya, pesa na gari.

Ripoti hiyo nayo haikutaja ni lini zimefanyika operesheni hizo wala uraia wa watu waliotiwa mbaroni lakini imethibitisha kuwa wawili ya watuhumiwa hao walikuwa wakisakwa kwa tuhuma mbalimbali.

Serikali ya Tunisia imechukua msimamo mkali dhidi ya magendo ya mihadarati na dawa haramu za kulevya. Hivi karibuni Tunisia imeanzisha operesheni kabambe za nchi nzima na kufanikiwa kukamata mamia ya watu wanaojihusisha na magendo ya madawa ya kulevya.

Mbali na magendo ya madawa ya kulevya, katikati ya mwezi uliopita wa Novemba, Walinzi wa Taifa wa Tunisia walitangaza kuwa wamesambaratisha mtandao wa magendo ya binadamu unaohusika na kusafirisha wahamiaji wasio na vibali.