Wahamiaji 499 waliokolewa katika pwani ya Libya wiki iliyopita
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa, wahamiaji 499, wakiwemo wanawake 34 na watoto sita, waliokolewa nje ya pwani ya Libya wiki iliyopita.
"Kuanzia Disemba 8 hadi 14, wahamiaji 499 waliokolewa na kurudishwa Libya," imesema taarifa hiyo ya IOM na kuongeza kuwa, wahamiaji 29 walitoweka na hawajapatikana hadi hivi sasa.
Kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, wahamiaji 21,343 wameokolewa na kurejea Libya, na hilo ni ongezeko la zaidi ya wahamiaji 4,000 ikilinganishwa na mwaka jana.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, IOM imerekodi vifo vya watu 635 na wahamiaji 982 waliopotea njiani baina ya Bahari Mediterania na maeneo yanayopakana na bahari hiyo, wakiwemo wale wanaotokea Libya na nchi nyingine.
Tangu mwaka 2011, wimbi la wahamiaji wanaotumia Bahari ya Mediterania kujaribu kuvuka upande wa pili kuelekea mwambao wa Ulaya limeongezeka mno.
Asilimia kubwa ya wahamiaji hao huwa hawafiki wanakokwenda. Wengi wao hufa maji na kuwa chakula cha wanyama wa baharini, wengine wanaishia kwenye mikono ya magenge hatari ya magendo ya binadamu, na wengine huishia kupigwa mnada na kuuzwa kama watumwa masokoni.