Afrika Kusini yaimarisha ulinzi kwenye mpaka wake na Msumbiji ili kuzuia jinai
(last modified Mon, 30 Dec 2024 12:22:28 GMT )
Dec 30, 2024 12:22 UTC
  • Afrika Kusini yaimarisha ulinzi kwenye mpaka wake na Msumbiji ili kuzuia jinai

Afrika Kusini imeimarisha ulinzi na doria kwenye mpaka wake na Msumbiji ili kuzuia na kupambana na uhalifu nyemelezi unaoweza kujitokeza kutokana na maandamano yanayoendelea katika nchi hiyo jirani.

Msumbiji imekumbwa na maandamano ya vurugu kwa wiki kadhaa sasa tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba; baada ya Tume ya  uchaguzi  ya nchi hiyo kumtangaza Daniel Chapo mwenye umri wa miaka 47 mgombea wa chama tawala cha Frelimo kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais.

Chapo aliibuka na ushindi wa asilimia 71 ya kura, na kumshinda mgombea wa upinzani Venancio Mondlane aliyepata asilimia 20.

Daniel Chapo, mshindi wa kiti cha urais Msumbiji 

Wapinzani wamepinga matokeo hayo ya uchaguzi wakidai kuwa matokeo ya uchaguzi yamechakachuliwa. Baraza la Katiba la Msumbiji ambalo lilipewa kazi ya kusimamia kesi hiyo wiki jana ilithibitisha kuwa Chapo ameshinda uchaguzi wa rais lakini likapunguza ushindi wa kura zake hadi asilimia 65. Hatua hii imeibua ghasia na machafuko mapya huko Msumbiji. 

Idara ya oparesheni za pamoja za kitaifa na intelijinsia ya Afrika Kusini imeeleza kuwa serikali ya nchi hiyo inaishirikisha kikamilifu serikali ya Msumbiji katika ngazi ya nchi mbili ili kupata ufumbuzi endelevu wa suala hili na kuimarisha hali ya usalama katika mikoa iliyoathirika huko Msumbiji. 

Mwezi uliopita, Afrika Kusini ilifunga kwa muda mpaka wake na Msumbiji kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji. Waandamanaji walichoma moto magari katika upande wa Msumbiji katika lango la kuingilia bandari ya Lebombo.