Naibu Rais wa Afrika Kusini: Afrika ijistawishe bila kutegemea Magharibi
Naibu wa Rais wa Afrika Kusini, Paul Mashatile amesema kuwa, bara la Afrika linapaswa kuhitimisha utegemezi wake kwa madola ya Magharibi.
Katika mahojiano na Russia Today, Mashatile ametoa wito wa mageuzi kwa taasisi za kimataifa na kueleza kuwa, Afrika Kusini na mataifa ya bara zima la Afrika lazima yatafute maendeleo huru na kuacha "kutegemea" Magharibi, haswa katika maeneo ya kiuchumi.
"Hatuwezi kuendelea kwa miaka na miaka tukitegemea Magharibi kwa maendeleo yetu sisi (watu wa nchi za) ulimwengu wa Kusini," Mashatile amesema.
Naibu Rais wa Afrika Kusini amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na mataifa yenye nguvu duniani, ikiwa ni pamoja na Marekani, lakini akasisitiza kwamba nchi za 'Kusini mwa Ulimwengu' lazima "ziwe na uhuru wa kujiendeleza."
Huko nyuma pia, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema mataifa ya bara hilo yanapaswa kushirikiana na kufanya kazi pamoja, ili kuhakikisha kuwa yanaondokana na utegemezi na vilevile yanajikomboa kifedha.
Alisema hatua ya umoja huo kutegemea ufadhili na fedha za misaada, inatishia uhuru wa taasisi hiyo kujitawala, kujiendeshea mambo yake namna inavyotaka na kujianishia mustakabali wake