Jeshi la Nigeria laangamiza magaidi 70 wa Boko Haram
Wizara ya Ulinzi ya Nigeria imesema wanamgambo wasiopungua 70 wa Boko Haram waliuawa katika msururu wa operesheni za karibuni za kijeshi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.
Katika taarifa, Mkurugenzi wa Habari wa wizara hiyo, Meja Jenerali Edward Buba amefichua kuwa, operesheni hizo zilifanyika kuanzia Januari 16 hadi 25 mwaka huu, katika eneo la Tumbuktu.
Meja Jenerali Edward Buba ameongeza kuwa, miongoni mwa wapiganaji waliouawa kwenye operesheni hizo ni makamanda watatu wa ngazi za juu wa kundi hilo la kigaidi.
Mkurugenzi wa Habari wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria pia amethibitisha habari za kuuawa wanajeshi 22 wa Nigeria wakati wa operesheni hizo, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Wakati huo huo, takriban wanajeshi 35 wa Nigeria wameripotiwa kuawa wakiwa kazini katika muda wa wiki tatu zilizopita, jambo linalodhihirisha changamoto kubwa zinazowakabili askari hao katika kupambana na ugaidi.
Vyanzo vya kijeshi na duru nyinginezo zimeiambia Anadolu kwamba, magaidi wanaoshirikiana na Daesh- Mkoa wa Afrika Magharibi (ISWAP) waliwaua takriban wanajeshi 20 wakati wa operesheni ya siku ya Ijumaa.
Boko Haram, ambayo imekuwa ikiendesha ugaidi nchini Nigeria tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, imehusika na mashambulizi makubwa ya kigaidi ambayo yameua makumi ya maelfu ya watu.