"Mapinduzi ya Kiislamu yaliathiri mapambano ya Afrika Kusini dhidi ya apartheid"
Mwanahabari mkongwe mjini Cape Town, Farid Sayed amesema Mapinduzi ya Kiislamu na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulikuwa na athari kubwa kwa mapambano ya Afrika Kusini dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid.
Katika mahojiano maalumu na Iran Press, Sayed amesema Mapinduzi ya Kiislamu yanaweza kutazamwa katika ngazi mbalimbali; katika muktadha wa Afrika Kusini na kimataifa, na pia umuhimu wake kwa watu wa Iran.
Amesema, kwa Afrika Kusini, baada ya mauaji ya halaiki ya Sharpeville wakati vuguvugu la ukombozi lilipopigwa marufuku, wengi walidhani mapambano hayo yamezimwa. "Hata hivyo," anaendelea kusema, "Mwamko wa Vijana Mwaka 1976 katika kitongoji cha Soweto ilikuwa chachu ya kushika kasi mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, huku wanafunzi na viongozi wakitafuta msukumo wa kimataifa kuendelea," amefafanua.
Mwanahabari huyo mashuhuri wa Afrika Kusini ameeleza kuwa: Ulimwengu pia ulitawaliwa na mataifa makubwa, Marekani na Umoja wa Sovieti. Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalidhihirisha uongozi wa kimapinduzi wa Imam Khomeini, na kujitolea bila woga kukabiliana na madola makubwa.

Amebainisha kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalitoa msukumo wa aina yake kwa mapambano mbali mbali kama vile ya Afrika Kusini dhidi ya apartheid, na kuwapa Waafrika Kusini ujasiri wa kupambana bila woga.
Sayed ameongeza kuwa, licha ya changamoto nyingi, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo katika nyanja za elimu na afya, na Afrika Kusini, kama demokrasia changa, inaweza kujifunza mambo mengi kutoka kwa Iran.