Waasi wa M23 waingia Bukavu baada ya kutwaa uwanja wa ndege
(last modified Sat, 15 Feb 2025 07:12:36 GMT )
Feb 15, 2025 07:12 UTC
  • Waasi wa M23 waingia Bukavu baada ya kutwaa uwanja wa ndege

Waasi wa M23 wametangaza habari ya kuingia katika jiji la Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mapema jana Ijumaa, jeshi la Kongo lilithibitisha kwamba wapiganaji wa M23 wamechukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa Kavumba, kaskazini mwa Bukavu, na kwamba wanajeshi wa Kongo walikuwa wamerudi nyuma na vifaa vyao.

Waasi hao wamekuwa wakijaribu kuelekea kusini upande wa Bukavu, tangu walipouteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Kongo, mwishoni mwa mwezi uliopita. "Ninathibitisha kwamba tuliingia Bukavu jioni hii (jana Ijumaa), na kesho (leo Jumamosi), tutaendelea na operesheni ya kusafisha jiji," amesema Corneille Nangaa, kiongozi wa Muungano wa Mto Kongo, unaojumuisha M23.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, amesema Kinshasa inatafuta "njia za kukabiliana" na Rwanda kutokana na kuongezeka taharuki na mapigano mashariki mwa DRC.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi

"Rwanda imekuwa ikichochea hali kama hizi mara kwa mara kwa miaka mingi, na hakujawa na hatua zozote za kukabiliana nazo," Tshisekedi ameambia jopo la mdahalo katika Mkutano wa Usalama wa Munich.

Hata hivyo akijibu madai hayo, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda amesema, “Kama tulivyosikia kutoka kwa jopo, mgogoro wa mashariki mwa DRC ni changamoto kwetu sote katika kanda. Rwanda imeathiriwa pakubwa na matokeo mabaya ya mgogoro huo kibinadamu, kisiasa na kiuchumi. Hata hivyo, Rwanda haipati faida yoyote kutoka kwa DRC isiyo na utulivu.”