Rwanda: Vikwazo vya Marekani si halali, havina msingi wowote
Serikali ya Kigali imelaani vikali hatua ya Wizara ya Hazina (Fedha) ya Marekani ya kumwekea vikwazo Waziri wa Utangamano wa Kieneo wa Rwanda, Jenerali (Mstaafu) James Kabarebe, kwa tuhuma za kuhusika na mzozo na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda imesema katika taarifa kuwa: Hatua ya kuwekewa vikwazo Waziri wa Serikali, Jenerali (Mstaafu) James Kabarebe haihalalishiki na wala haina msingi wowote.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza bayana kuwa, "Iwapo vikwazo vingeweza kutatua mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tungelikuwa na amani katika eneo miongo kadhaa iliyopita."
Aidha taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda imeikosoa jamii ya kimataifa kwa kutochukua hatua za kivitendo za kujaribu kuzima mgogoro wa ukosefu wa usalama na ghasia mashariki mwa Kongo, unaochochewa na serikali ya DRC.
Mbali na Jenerali (Mstaafu) Kabarebe, Marekani imemuwekea vikwazo pia msemaji wa kundi la waasi wa M23, Lawrence Kanyuka, pamoja na kampuni nyingine mbili zinazodaiwa kufadhili na kuchochea mapigano mashariki ya DRC.
Wakati huo huo, Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) vimeelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya hali mbaya ya mzozo wa kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hasa katika jimbo la Kivu Kusini.

Mkurugenzi Mkuu Jean Kaseya aliuambia mkutano wa waandishi wa habari jana Alkhamisi kwa njia ya mtandaoni kwamba,“Tunacheza na moto; ikiwa hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haitatatuliwa, pamoja na kusimamishwa kwa ufadhili wa Marekani, tutashuhudia DR Congo ikigeuka kuwa kitovu cha mripuko mkubwa wa janga ambalo linaweza kuenea nje ya jimbo hilo hadi nchi zingine zilipo karibu na eneo hilo."
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, tangu Januari 26, mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000, majeruhi 3,000, na zaidi ya watu 500,000 kuhama makazi yao, mbali na watu milioni 6.4 ambao tayari walikuwa wamekimbia makazi yao.