Rais Tshisekedi anapanga kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
-
Felix Tshisekedi
Rais wa Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anatazamiwa kuzindua serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Tina Salama, msemaji wa Ofisi ya Rais wa Kongo amesema, Rais Tshisekedi ataunda serikali ya umoja wa kitaifa na kufanya mabadiliko ya uongozi katika muungano tawala wa nchi hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameeleza mpango wake huo wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kufuatia mashinikizo ya ndani kutokana na jinsi alivyoshughulikia mashambulizi ya waasi wa kundi la M23 katika majimbo ya mashariki mwa nchi hiyo.
Rais wa Kongo ametangaza kuwa atajielekeza kwenye serikali ya umoja wa kitaifa na kufanya mabadiliko ndani ya uongozi wa Muungano Mtakatifu wa nchi hiyo.
Rais Felix Tshisekedi ameueleza mkutano wa Muungano Mtakatifu wa serikali mseto inayoongoza ya Kongo kwamba hawapaswi kuyumbishwa na mivutano ya ndani na amesisitiza udharura wa kuungana kwa ajili ya kukabiliana na adui.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2025, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaendelea kukumbwa na majanga mtawalia katika majimbo ya Kaskazini na Kusini mwa nchi hiyo.
Herve Diakiese kiongozi wa upinzani amekosoa namna Rais Tshisekedi anavyoiendesha nchi akisema suala hilo ni miongoni mwa sababu za mgogoro wa sasa nchi hiyo.
Hatua ya kundi la waasi wa M23 ya kuyadhibiti maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo na akiba ya madini ya thamani kubwa imeibua wasiwasi wa kujiri vita vikubwa huku baadhi ya wanachama wa mirengo ya upinzani wakitabiri wazi kuwa Rais Felix Tshikesedi hatosalia madarakani kwa muda mrefu kufuatia hali hii ya sasa.

Rwanda ambayo inatuhumiwa kuwasaidia waasi wa M23 imekanusha suala hilo ingawa Rais Kagame wa nchi hiyo anasisitiza kuwa waasi hao wanastahili kuungwa mkono.
Kagame amesisitiza kuwa juhudi zozote za kumaliza mzozo huo lazima zishughulikie masuala ya usalama yanayotokana na ukiukwaji wa sheria mashariki mwa Kongo pamoja na ubaguzi unaoendelea dhidi ya Watutsi wa Kongo.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa wanajeshi karibu 4,000 wa Rwanda wanawasaidia wanamgambo wa M23.