Hujuma za waasi mashariki mwa Kongo zimeuwa watu 7,000 mwaka huu
(last modified Tue, 25 Feb 2025 02:30:05 GMT )
Feb 25, 2025 02:30 UTC
  • Hujuma za waasi mashariki mwa Kongo zimeuwa watu 7,000 mwaka huu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa watu zaidi ya elfu saba wameuawa mwaka huu wakati waasi wa kundi la M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakiteka miji kadhaa katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo.

Judith Suminwa ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa hali ya usalama na kibinadamu mashariki mwa Kongo imefikia kiwango cha kutisha.

Mzozo wa mashariki mwa Kongo ulishika kasi hivi karibuni, wakati waasi walipouteka mji wa Goma mwezi Januari mwaka huu na kisha Bukavu makao makuu mengine ya kijimbo.

Jana Jumatatu ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda, kufuatilia matukio yanayoendelea kujiri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuchukua hatua zinazohitajika za kukabiliana na mgogoro huo.

Wakati huo huo, Muungano wa waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Alliance Fleuve Congo (AFC), unaojumuisha waasi wa M23, umetangaza kuwa uko tayari kushiriki mazungumzo na serikali ili kusitisha mara moja mapigano mashariki mwa nchi. Haya yameelezwa na msemaji wa kundi hilo.