Mgogoro mashariki mwa DRC waathiri zaidi ya wanafunzi milioni 1
(last modified Thu, 27 Feb 2025 11:02:25 GMT )
Feb 27, 2025 11:02 UTC
  • Mgogoro mashariki mwa DRC waathiri zaidi ya wanafunzi milioni 1

Kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo waasi wa M23 wameshadidisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali, kumesababisha shule 2,594 kufungwa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Elimu ya DRC inasema kuwa, shule 1,483 zimefungwa katika jimbo la Kivu Kaskazini huku nyingine 1,111 zikifungwa katika jimbo la Kivu Kusini, na kuathiri watoto milioni 1.1.

"Kurejeshwa kwa shughuli za shule kumekuwa kugumu, huku usalama wa wanafunzi na walimu ukiwa hatarini kutokana na mada za miripuko katika baadhi ya shule," wizara hiyo imesema.

Wizara ya Elimu ya DRC imesema, “Shule nyingi zimeshambuliwa kwa mabomu, kuharibiwa au kubadilishwa kuwa kambi za kijeshi na makundi yenye silaha. Kwa kulenga wanafunzi na shule, vita hivi pia ni vita dhidi ya mustakabali wetu."

Katika mkasa ambao haujawahi kushuhudiwa, shule moja iligeuzwa kuwa kaburi, jambo linaloonyesha hali ya kutisha na kukata tamaa ambayo inakumba sekta ya elimu katika maeneo yenye migogoro,” imeongeza taarifa hiyo.

Waasi wa kundi la M23

Kundi la M23 limezidisha udhibiti wa eneo la mashariki mwa Kongo DR tangu Disemba mwaka uliopita, na kutwaa miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu.

Mapigano mashariki mwa Kongo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 7,000 mwaka huu, Waziri Mkuu wa DRC, Judith Suminwa Tuluka aliambia Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu.