Afrika Kusini yapinga 'diplomasia ya kipaza sauti' na ya kibabe ya Trump
(last modified Mon, 10 Mar 2025 07:01:30 GMT )
Mar 10, 2025 07:01 UTC
  • Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
    Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini

Huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiendelea kuingilia masuala ya ndani ya Afrika Kusini, serikali ya Pretoria imetangaza kwamba haitajihusisha na diplomasia isiyojenga ya "ya kipaza sauti" na ya bwabwaja ya Marekani.

Msimamo huu wa serikali ya Afrika Kusini umetangazwa baada ya Donald Trump kutuma ujumbe kwa mara nyingine kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa serikali ya Pretoria inawanyang'anya watu weupe ardhi yao. Trump pia alidai kuwa Marekani iko tayari kutoa uraia wa Marekani kwa wakulima wazungu wa Afrika Kusini ambao amedai wanapokonywa ardhi yao.

Serikali ya Afrika Kusini imesisitiza kuwa, Rais wa Marekani ana dhana potofu kuhusu sheria mpya ya ardhi nchini Afrika Kusini.

Pretoria imesema: Wasiwasi wa Trump kuhusu kunyang'anywa ardhi wakulima wazungu sio sababu ya kukata misaada kwa Afrika Kusini, bali sababu kuu ni Trump kuchukizwa na hatua za serikali ya Pretoria na harakati zake za kisheria dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Afrika Kusini imesisitiza kuwa, licha ya vitisho vya serikali ya Marekani, haitaondoa malalamiko yake dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kwa hali yoyote ile.

Hivi karibuni pia Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Ronald Ramola, alisisitiza katika mahojiano na Financial Times kwamba: "Wakati mwingine kushikamana na misingi na kanuni kuna athari zake, lakini tunasimama kidete kwa sababu ni muhimu kwa dunia na utawala wa sheria."

Ronald Ramola

Itakumbukwa kuwa, Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza kuwasilisha mashtaka dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kutokana na uhalifu wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala huo ukisaidiwa na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kama Ujerumani dhidi ya watu wa Gaza.