Nigeria yathibitisha vifo vipya vitano kutokana na homa ya Lassa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123834-nigeria_yathibitisha_vifo_vipya_vitano_kutokana_na_homa_ya_lassa
Nigeria imethibitisha vifo vipya vitano kutokana na homa ya Lassa, ugonjwa ambao umesambaa katika eneo la magharibi mwa Afrika.
(last modified 2025-03-13T02:21:46+00:00 )
Mar 13, 2025 02:21 UTC
  • Nigeria yathibitisha vifo vipya vitano kutokana na homa ya Lassa

Nigeria imethibitisha vifo vipya vitano kutokana na homa ya Lassa, ugonjwa ambao umesambaa katika eneo la magharibi mwa Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nigeria (NCDC), jumla ya vifo vilivyoripotiwa mwaka huu vimefika 100.

Kituo hicho kimeeleza kuwa, kimekuwa kikifuatilia kwa karibu hali ya mambo na kwamba takwimu zinaonyesha ongezeko la vifo vilivyosababishwa na homa ya Lassa.

Ripoti iliyotolewa jana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nigeria (NCDC) mbele ya waandishi wa habari ilibainisha kuwa kituo hicho kimesajili watu wengine 236 wanaoshukiwa kuambukizwa homa hiyo, kesi mpya 29 zilizothibitishwa na vifo vitano kutoka majimbo 13 ya nchi hiyo. 

Nigeria CDC imeongeza kuwa: Kwa ujumla, kwa mwaka huu majimbo 13 yamesajili angalau mgonjwa mmoja aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo miongoni mwa maeneo 75 ya serikali za mitaa. 

Ugonjwa wa homa ya Lassa kwa kawaida huenezwa kwa kugusana na panya walioambukizwa, chakula kilichochafuliwa, au wahudumu wa afya ambao hukutana na wagonjwa walioambukizwa. Mgonjwa anaweza kudhihirisha dalili kuanzia kuwa na homa ya wastani hadi kali ikiwa ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa na ya misuli.