Rais Yoweri Museveni: Kuna haja kwa Uganda kujitoa katika mahakama ya ICC
Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amesema kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imegeuka na kuwa silaha iliyo dhidi ya bara la Afrika.
Rais Museveni ameelezea kusikitishwa kwake na jinsi mahakama hiyo ya kimataifa yenye makao yake huko The Hague Uholanzi inavyotumiwa na madola ya Magharibi kama silaha dhidi ya Afrika. Rais Museveni anayetarajiwa kuwania tena kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa mwezi huu amesema kuwa, kuna udharura kwa Uganda kujitoa katika mahakama hiyo. Amesema kuwa, mahakama hiyo haifanyi kazi zake kwa uadilifu na kwamba kuna watenda jinai wengi mno ambao wanapaswa kutiwa mbaroni na kushtakiwa na mahakama ya ICC lakini mahakama hiyo haifanyi hivyo na badala yake imekuwa ikiwaandama tu viongozi wa Kiafrika. Hayo yanajiri katika hali ambayo, weledi wengi wa mambo wamekuwa wakiikosoa vikali mahakama hiyo wakisema kwamba, inatumiwa kisiasa na madola ya kibeberu kwani wanaoandamwa zaidi na mahakama hiyo ni viongozi wa Kiafrika.
Katika siku za hivi karibuni, viongozi mbalimbali wa Kiafrika wamekuwa wakisisitiza juu ya udharura wa bara la Afrika kujitoa katika mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo.
Ikumbukwe kuwa, katika mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika hivi karibuni mjini Addis Ababa Ethiopia, mpango uliowasilishwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wa kujitoa bara hilo katika mkataba huo uliungwa mkono na mkutano huo.