Rais wa Tunisia amfuta kazi Waziri Mkuu, Kamel Maddouri
-
Kais Saied
Rais wa Tunisia, Kais Saied amemfukuza kazi Waziri Mkuu, Kamel Maddouri na kumteua Waziri wa Vifaa na Makazi, Sara Zaafarani kushika nafasi yake.
Hayo yametangazwa na Ofisi ya Rais wa Tunisia mapema leo Ijumaa, bila kutoa maelezo yoyote kuhusu hatua hiyo.
Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Kitaifa, ambayo imechapishwa na Ofisi ya Rais wa Tunisia, Kais Saied amesema: Tutaendeleza mapambano ya ukombozi hadi raia wote wapate haki. Tutaendelea kuzuia njama zote zinazofanywa dhidi ya Serikali ya Tunisia."
Sara Zaafarani, mhandisi ambaye amehudumu kama Waziri wa Vifaa na Nyumba tangu 2021, anakuwa waziri mkuu wa tatu wa Tunisia katika kipindi cha chini ya miaka miwili.
Katika miezi ya hivi karibuni Saied amekuwa akikosoa utendakazi wa mawaziri wa serikali yake mara kwa mara akisema utendakazi wao haujakidhi viwango vinavyotakiwa na matarajio ya wananchi wa Tunisia ni makubwa.
Mwezi uliopita, alimfukuza kazi Waziri wa Fedha, Sihem Boughdiri.
Saied, ambaye alichaguliwa Oktoba 2019, alihodhi mamlaka yote ya nchi miaka mitatu iliyopita, akamfukuza waziri wake mkuu wakati huo na kusimamisha Bunge, ambalo baadaye lilivunjwa kabisa.
Wapinzani wake, husuasan chama kilichopigwa marufuku cha Ennahda, wanamtuhumu kuwa amefanya mapinduzii baridi nchini humo.