Netumbo Nandi aapishwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia
(last modified Fri, 21 Mar 2025 14:42:52 GMT )
Mar 21, 2025 14:42 UTC
  • Nandi-Ndaitwah
    Nandi-Ndaitwah

Netumbo Nandi Ndaitwah ameapishwa leo Ijumaa kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia, baada ya kushinda uchaguzi mwaka jana.

Nandi-Ndaitwah, mwenye miaka 72, amekuwa mmoja wa viongozi wachache wanawake barani  Afrika, kufuatia sherehe ya uapisho iliyofanyika leo na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Angola, Afrika Kusini na Tanzania. 

Rais anayeondoka madarakani wa Namibia, Nangolo Mbumba mwenye umri wa miaka 83, amemkabidhi madaraka Rais mpya, Nandi- Ndaitwah, katika sherehe zilizokwenda sambamba na maadhimisho ya mwaka wa 35 wa uhuru wa Namibia. Mvua kubwa zilizonyesha leo zilipelekea kuhamishwa shamrashamra za hafla hiyo kutoka uwanja wa uhuru hadi katika Ikulu ya Rais.

Makofi na vifijo vilisikika wakati wa kula kiapo Rais mpya wa Namibia, Nandi-Ndaitwah.

Akihutubia katika hafla hiyo, Nandi-Ndaitwah amesema kuwa ameweka historia kufuatia kuchaguliwa kwake kuiongoza Namibia na kwamba wananchi walimchagua kutokana na umahiri na sifa zake. 

 Amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanywa licha ya Namibia kupiga hatua katika baadhi ya mambo tangu ipate uhuru. 

Itakumbukwa kuwa, Rais mpya wa Namibia ambaye awali alikuwa Makamu wa Rais kwa muda wa mwaka mmoja, ni mwanchama wa siku nyingi wa chama cha SWAPO ambacho kimeiongoza nchi hiyo yenye idadi ndogo ya watu lakini yenye utajiri wa madini ya urani kupata uhuru wake mwaka 1990.