Sakata la uuzaji wa Msikiti mkongwe zaidi Kenya
(last modified Sun, 06 Apr 2025 02:29:06 GMT )
Apr 06, 2025 02:29 UTC
  • Sakata la uuzaji wa Msikiti mkongwe zaidi Kenya

Msikiti wa kihistoria wa Kongo, ulioko Diani, Kaunti ya Kwale, umekuwa katika mzozo baada ya mwekezaji binafsi kudai umiliki wa ardhi hiyo na kupewa hatimiliki mnamo Februari 17, 2025.

Jamii ya Waislamu nchini Kenya, kupitia wakili wao Paul Mwangi, imewasilisha malalamiko kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), wakitaka uchunguzi ufanywe kuhusu uhalali wa utoaji wa hatimiliki hiyo. Wanasisitiza kuwa faili la mahakama lililohusiana na kesi hiyo pia limepotea, jambo linalozua maswali kuhusu uhalali wa mchakato huo.

Katika barua kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Abdi Mohammed, wakili Mwangi amesema kuwa, ingawa msikiti huo wa kihistoria upo kwenye ardhi ya umma, hatimiliki hiyo ilitolewa kwa watu wawili binafsi mnamo Februari 17, 2025.

Wakili Mwangi anasema kuwa mapema mwaka huu, ardhi hiyo pia ilitangazwa kuuzwa kwa Shilingi bilioni 1.4 na watu waliokabidhiwa umiliki wake mnamo 2005 kupitia uamuzi wa mahakama.

Katika barua yake, anasisitiza kuwa msikiti huo ni mnara wa kihistoria unaolindwa kisheria.

Taarifa zaidi zinasema kuwa Gavana wa Kaunti ya Kwale, Bi. Fatuma Achani, amesitisha uuzaji wa ardhi ya msikiti huo ulioko katika eneo la Msambweni.

Kupitia akaunti yake ya Facebook, Gavana Achani amesema ameweka vikwazo vya kutouzwa (caveat) kwa ardhi hiyo katika ofisi za ardhi, kutokana na umuhimu wake kwa jamii inayomiliki msikiti huo – ambao unasemekana kuwa mkongwe zaidi katika historia ya Uislamu nchini Kenya.

Inasemekana kuwa ardhi hiyo hapo awali ilimilikiwa na marehemu Rais Daniel Arap Moi, ambaye aliirejesha hatimiliki hiyo mnamo 2009 baada ya kugundua kuwa aliipata kwa njia isiyo halali kutoka kwa Kamishna wa Ardhi wa wakati huo mnamo 1986.

Msikiti wa Kongo unachukuliwa kuwa mnara wa kihistoria na sehemu ya urithi wa kitamaduni wa Kenya. Jamii ya Waislamu inasisitiza kuwa ardhi hiyo ni mali ya umma na kwamba msikiti huo unapaswa kulindwa kisheria.

Hapo awali, msikiti huo ulijulikana kama Msikiti wa Uajemi wa Diani – jina lililotokana na Wafanyabiashara kutoka Uajemi (Iran) waliokuwa wakiishi eneo hilo wakati wa ujenzi wake katika karne ya 14 Miladia.