Mwangwi wa hasira za wananchi wa Morocco dhidi ya jinai za Israel
(last modified Tue, 08 Apr 2025 11:55:24 GMT )
Apr 08, 2025 11:55 UTC
  • Mwangwi wa hasira za wananchi wa Morocco dhidi ya jinai za Israel

Maelfu ya wananchi wa Morocco wamefanya maandamano huko Rabat, mji mkuu wa nchi hiyo wakilaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza na kutaka kufutwa makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida kati ya Morocco na utawala wa Kizayuni.

Katika maandamano hayo ambayo yametajwa kuwa ni miongoni mwa maandamano makubwa ya wananchi wa Morocco dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni; maelfu ya raia wa nchi hiyo walisafiri kutoka kona mbalimbali za Morocco na kuelekea Rabat wakitoa mwito kwa viongozi wa nchi hiyo kuiunga mkono Palestina na kupinga uhusiano na utawala wa Kizayuni.

Washiriki wa maandamano hayo sambamba na kulaani jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza, wametoa mwito wa kukomeshwa mara moja uhusiano wa nchi yao na Israel.

Maandamano ya "Hands Off" ya nchini Marekani ya kuliunga mkono taifa la Palestina na kupinga udikteta wa Trump

 

Makubaliano ya kuweko uhusiano wa kawaida kati ya Morocco na utawala wa Kizayuni yalifikiwa mwezi Disemba 2020. Marekani iliiahidi Morocco kuwa italitambua eneo la Sahara Magharibi kuwa ni milki ya Morocco kwa sharti kwamba utawala wa kifalme wa nchi hiyo uwe na uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Kizayuni. Uamuzi huo wa kisiasa wa serikali ya Morocco ulikuwa unasubiri kisingizio tu kwa sababu viongozi wa nchi hiyo walikuwa muda mrefu wanajaribu kuunganisha msimamo wao wa kidiplomasia na kikanda kupitia makubaliano kama hayo ili wapate msaada wa kiuchumi na kijeshi wa Marekani. Maafisa wa Morocco pia walitumai kuwa Israel ingeisaidia nchi hiyo katika nyanja mbalimbali hususan teknolojia, kilimo na usalama wa kijeshi, matumaini ambayo si tu hayakutimia bali pia yameendelea hadi leo kuzusha maandamano ya umma dhidi ya utawala wa kifalme wa Morocco. Tangu kutiwa saini mkataba huu, wananchi wa Morocco ambao wana mizizi mirefu ya Kiislamu na Kiarabu na wamejikita kwenye kuliunga mkono taifa la Palestina, wameonesha mara kwa mara upinzani wao dhidi ya maamuzi ya watawala wa nchi hiyo kupitia kufanya mikutano mikubwa huko Rabat na kwenye miji mingine.

Maandamano hayo yameshika kasi katika miaka michache iliyopita hususan tangu kuanza Vita vya Ghaza na jinai kubwa zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wananchi wa Morocco mbali na kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, mara kadhaa wametoa mwito wa kufutwa makubaliano ya kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni.

Uungaji mkono wa Palestina umo ndani ya damu za wananchi wa Morocco

 

Kwa mtazamo wa Waislamu wa Morocco, makubaliano hayo na Israel ni usaliti kwa kadhia ya Palestina na ni kuungana na wavamizi makatili.

Kwa mara nyingine tena maandamano makubwa yameanza nchini Morocco na katika nchi nyingi zinazounga mkono kadhia ya Palestina kuanzia Indonesia na Malaysia hadi Misri kufuatia Israel kuvunja makubaliano ya kusitisha vita na Hamas. Kwa watu wa Morocco, Palestina ni suala la ulimwengu wa Kiislamu, hivyo kuwa na uhusiano wowote na utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu ni usaliti wa sheria za kimsingi za dhamiri ya kibinadamu ya kila Muislamu.

Maandamano ya wananchi wa Morocco dhidi ya makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel yanaonesha kwamba wananchi hao wanataka kuiona nchi yao inaliunga mkono taifa la Palesstina na kwamba raia wako macho na hawajadanganywa na maneno kama vile "amani," "maendeleo ya kiuchumi" au "usalama wa kikanda" yanayotumiwa kujaribu kuhalalisha makubaliano na Israel. 

Hali ilivyo inakwenda mkondo tofauti na zilivyotarajia propaganda za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa nchi za Magharibi wanaojaribu kuwaonesha wananchi wa Morocco kuwa eti nchi hiyo imenufaika kwa kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel. Ushahidi wa hayo ni pale wanapoonekana waandamanaji wengi wa Morocco wakiwa wamebeba mabango katika mikutano ya hadhara na maandamano, yenye maandishi yanayosema: "Mauti kwa Uzayuni" au "Palestina itakombolewa."

Maandamano ya Wamarekani dhidi ya Trump

 

Ijapokuwa jinai za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zimekuwepo kwa miaka mingi, lakini hivi sasa hisia za wanadamu katika kona zote za dunia zimeamka zaidi kutokana na operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na mapambano ya kishujaa ya makundi ya Muqawama ya Ghaza kwa kushirikiana na makundi mengine ya Muqawama nje ya Palestina kama vile Lebanon, Iraq na Yemen. Hivi sasa mwangwi wa hasira ya kimataifa dhidi ya jinai za Wazayuni unasikika kila mahala. Maandamano ya mamilioni ya watu katika majimbo 50 ya Marekani na katika nchi mbalimbali tofauti chini ya kaulimbiu ya "Hands Off" kulalamikia kushiriki Marekani kwenye jinai za Israel huko Ghaza, ni ushahidi wa wazi wa kuamka zaidi hisia za walimwengu na kutambua uhakika wa mambo kuhusu madola ya kibeberu duniani.