Makumi wauawa katika shambulio la wabeba silaha Nigeria
Zaidi ya watu 40 wameuawa katika shambulio la usiku wa manane dhidi ya jamii ya Zike huko Bassa, Jimbo la Plateau, huku mashambulio makali ya makundi yenye silaha yakiendelea kuripotiwa katika eneo hilo la kaskazini ya kati mwa Nigeria.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya ndani vilivyozungumza na shirika la habari la Anadolu, shambulio hilo ambalo lilianza usiku wa manane Jumatatu, lilidumu kwa karibu saa mbili,
Zaidi ya watu 40 wamethibitishwa kuuawa, huku karibu wakazi 1,000 wakiyakimbia makazi yao, kwa mujibu wa Joseph Chudu Yonkpa, Katibu Taifa wa Uenezi wa Harakati ya Vijana ya Irigwe.
Yonkpa ameongeza kuwa, akthari ya watu waliojeruhiwa wanapokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Jos na vituo vingine vya matibabu vilivyo karibu.
Naye Alfred Alubo, Msemaji wa Kamanda wa Polisi wa Jimbo la Plateau, amethibitisha tukio hilo lakini alisema idadi kamili ya waliouawa na kujeruhiwa bado haijajulikana. Amesema taarifa rasmi itatolewa mara baada ya kukusanyawa maelezo kamili ya shambulio hilo.
Jamii ya Zike imekumbwa na wimbi la mashambulizi makali katika wiki za hivi karibuni, huku zaidi ya watu 20 wakiuawa katika matukio tofauti kabla ya shambulio la jana Jumatatu.
Haya yanajiri siku moja baada ya watu wanane kuuawa na wengine 11 kujeruhiwa wakati basi moja katika Jimbo la Borno nchini Nigeria, kaskazini mashariki mwa Nigeria lilipokanyaga bomu lililotegwa ardhini na magaidi wa Boko Haram.