Magaidi 21 wauawa magharibi mwa Mali
Jeshi la Mali limetangaza kuwa limeua magaidi 21 wakati wa operesheni zake kwenye eneo la Sebabougou la magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Taarifa ya Jeshi la Mali ya jana Jumatatu imesema: "Sebabougou sasa iko chini ya udhibiti wa jeshi kutokana na mashambulizi ya anga yaliyolenga maficho ya magaidi na kuharibu kambi zao kadhaa."
Taarifa hiyo pia imesema: "Wakati magaidi hao walipokimbia, waliacha nyuma yao maiti 21, makumi ya silaha, risasi na zana za kijeshi pamoja na magari na vifaa vya mawasiliano."
"Operesheni za msako zinaendelea dhidi ya wahalifu wengi waliojeruhiwa na waliokimbia," imesema taarifa ya jeshi la Mali na kuongeza kuwa askari watano walijeruhiwa wakati wa mapigano hayo.
Tukumbuke kwamba mwezi Februari mwaka huu, Jeshi la Mali liliahidi kuwasaka magaidi waliohusika na shambulio la kikatili dhidi ya msafara mkubwa uliokuwa unakwenda kwenye mgodi wa dhahabu nchini humo.
Maafisa wa Mali walieleza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo na wengine kadhaa kutoka kundi la Wagner walikuwa wakilisindikiza kundi la watu ambao wengi walikuwa ni raia wa kigeni kuelekea katika mgodi wa madini wa Intahaka ambalo ni eneo kuu la uchimbaji dhahabu kaskazini mwa Mali wakati walipovamiwa ghafla na watu waliokuwa na silaha.
Afisa wa ngazi ya Jenerali wa jeshi la Mali ambaye hakutaka jina lake litajwe aliviambia vyombo vya habari kuwa magaidi waliwashambulia kwa makusudi raia wa kawaida wakati na kwamba wanaendelea kuwasaka magaidi waliohusika na mauaji ya raia hao. Mali ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa madini ya dhahabu barani Afrika, ingawa uzalishaji umeshuka kutokana na ukosefu wa usalama.